contact

husen

Thursday, May 24, 2012

NCHUNGA ABWAGA MANYANGA

Ndugu wana Habari, najua kwamba taarifa hii itawafedhehesha wajumbe
 na wanayanga wanaotuunga mkono,hasa ukizingatia maamuzi ya 
pamoja ya vikao vyetu vya kamati ya utendaji vilivyopita kwamba
 hakuna wa kujiuzulu kati yetu mpaka tujue hatma ya mkutano mkuu
 ambao tulipanga ufanyike tarehe 15 Julai 2012, ukiachia mbali
 shinikizo la kujiuzulu linalotolewa na baadhi ya wazee na
 wanaojiita vijana wa klab, kwa wajumbe wa kamati ya utendaji,
 na hasa mimi kama mwenyekiti.
Nawashukuru wajumbe kwamba tulifanya kazi kwa pamoja na 
kwa ushirikiano mzuri, na hata pale tulipotofautiana tulifanya
 hivyo kwa hoja na kufikia maazimio ambayo wote tulikuwa
 tunawajibika nayo.
Tangu tumeingia madarakani tumeweza kushirikiana na 
kupata mataji matatu katika kipindi cha mwaka mmoja,
 yaani; Ngao ya Hisani 2010, Ubingwa wa ligi kuu ya Vodacom
 2010/2011, na Ubingwa wa  Afrika Mashariki na Kati (Kagame Cup), 2011.
 Zaidi ni kwamba tuliuwa uteja kwa watani wetu wa jadi kila
 tulipokutana katika ligi ukiachia mbali mechi ya tarehe 6 Mei 2012, 
ambayo tulifungwa goli 5 bila, na kuleta mtafaruku mkubwa katika klab yetu.
Hali kadhalika tumeshirikiana  mpaka tumeweza kuboresha 
mkataba kati yetu na TBL kupitia Kilimanjaro Premium Lager,
 tumeingia mkataba na  kampuni ya NEDCO  kuendeleza mali 
zetu katika mtaa wa mafia na uwanja wetu wa KAUNDA baada
 ya kufikia hatua nzuri katika kupata hati miliki za maeneo
 yote mawili. Nafahamu kwamba kampuni hiyo iko katika hatua
 za mwisho za kumalizia michoro.
Hali kadhalika tuliingia mkataba wa kuzalisha na kuuza bidhaa
 zenye nembo yetu na hasa baada ya kufanya marekebisho
 yatokanayo na matakwa ya sheria kule BRELA na pia mkataba
 na kampuni ya NEXUS LTD, ambayo itakuwa inatutafutia
 wadhamini wa nje na ndani, kufanya promosheni zetu na
 kampeni kwa njia ya electronic kupitia mitandao mbalimbali
 na kukusanya data za wanachama na kusajili  wapya tukiwa
 na malengo ya kukusanya shilingi 300,000,000/= hadi 800,000,000/=
 kwa mwaka katika kipindi cha miaka mitatu. Haya yote tuliyafanya
 tukilenga kujitegemea kujazia mapengo yaliyokuwa
 yakitokana na kutegemea ufadhili wa mtu mmoja mmoja.
Kwa ridhaa yenu tumekua tukiendelea na mazungumzo
 na makampuni mbali mbali kwa ajili ya udhamini na kwa
 sababu maalum, nitazitaja katika hati ya makabidhiano
 kwa kiongozi ajaye.
Aidha, tumeshirikiana katika kufanya mambo mbali mbali
 ya kijamii, ikiwa ni pamoja na sikukuu ya kuadhimisha
 miaka 77 ya Yanga, sikukuu za pasaka, kuchangia jamii na
 waliokumbwa na maafa, na kongamano la vijana lililolenga
 kuwaamsha vijana kuitambua nafasi yao katika Yanga ikiwa
 ni pamoja na kupata azimio la kuanzisha SACCOSS ya
 Yanga, ambapo maombi yapo kwa msajili Manispaa ya Ilala.
Haya yote nayataja ikiwa ni kuwashukuru kwa ushirikiano 
na ikiwezekana muweze kuyakamilisha yaliyobaki ambayo
 mtaona yalikuwa mazuri.
Lakini pia tulipopata matatizo tulikuwa pamoja.  Nichelee 
kusema tu kwamba tulisimama pamoja baada ya kujiuzulu
 Makamu Mwenyekiti wetu Ndugu Davis Mosha na mjumbe
 wetu  ndugu Seif A. Seif, Ali Mayayi, na wengineo, kwani
 tulifungwa na katiba.Tulisimama pamoja pia katika suala
 la kujiuzulu ndugu Yusuf M. Manji, aliyekuwa mdhamini 
mteule na mfadhili mkuu ambaye sasa ameonyesha nia ya
 kurudi nanyi mkaridhia mkutane naye. Awali, tulitumia 
kila jitihada za kumrejesha lakini ikashindikana.
Hata hivyo doa limetupata baada ya kufungwa na watani wetu
 goli 5 bila, ambapo kuna wanachama wanaoelewa na wasioelewa kabisa.
Ninachokiona mimi ni usaliti wa hali ya juu uliombatana na
 matukio mbalimbali yaliyopita na yanayoendelea hadi kujaribu
 kupindua uongozi wa halali wa kidemokrasia.
 SIWATUHUMU WACHEZAJI MOJA KWA MOJA, isipokuwa 
 mfululizo wa matukio wiki tatu kabla ya mchezo ule na sasa,
 inaonyesha kwamba kulikuwa na usaliti mkubwa ambao 
sisi hatukuweza kuubaini mapema.
Sioni mantiki katika hoja kwamba wachezaji walikuwa
 wakidai mishahara, posho n.k.  Au ati mtendaji wetu 
alishikiliwa Arusha kwa deni la hoteli, ndiyo  tuvune bao 5!
Kwa wanaoijua Yanga, imewahi kuwa na madeni makubwa
 katika Hoteli mbali mbali, mawakala wa ndege n.k, na baadhi
 tumeyakuta na sisi tumekuja tukayalipa. Hii imewahi kutokea 
kabla na wakati akiwepo mfadhili, sembuse sisi tulioachwa baki,
 na bado wachezaji walicheza kwa morali.
Hata hivyo, utamaduni wa kutimuana baada ya matokeo mabaya
 ni dhambi ambayo itatula kama hatutaiacha, kwani wenye
 hila na uchu wa madaraka wataendelea kutumia mbinu hiyo
 ili kuuondoa uongozi wa kidemokrasia.
Baada ya mapinduzi kushindikana na TFF kuonya kuhusu
 mapinduzi hayo, wazee kupitia msemaji wao , Mzee
 Akilimali wamesikika katika kipindi cha Michezo  cha Redio
 moja maarufu hapa nchini wakidai kwamba ni bora Yanga
 ishushwe daraja au kufungiwa kuliko mimi kuendelea kuongoza!
Hii imenikumbusha HEKMA ZA MFALME SELEMANI
 akiamulia ugomvi wa wanawake wawili waliokuwa wakigombea
 mtoto naye akaamuru wamgawane nusu kwa nusu. Yule 
mwenye mtoto kweli alimuomba Mfalme amuachie
 mwenzie kuliko kumkata nusu.
Kwa hekma hiyo nimeamua kujiuzulu nafasi yangu 
katika Uenyekiti  wa Yanga kwani ni klab ninayoipenda
 hata kama sio kiongozi kwa mujibu wa ibara ya 28 ya katiba yetu.
Vile vile siko tayari kuona klab yangu ikisalitiwa au
 kuhujumiwa eti kwa sababu tu mimi ni kiongozi.
Natumaini kamati ya utendaji kwa pamoja na wale
 tuliowateua chini ya ibara ya 29(3) ya katiba ya Yanga
 pamoja na bodi ya wadhamini, itawaongoza wanachama 
mpaka kufikia mkutano mkuu kwa  mafanikio zaidi.
 Nitaendelea kuwa mwanachama mwadilifu na nitatoa mchango 
wangu wa hali na mali pale nitakapo hitajika na nikiwa 
 na uwezo wa kufanya hivyo.
YANGA DAIMA MBELE, NYUMA MWIKO.
Wasalaam,
LLOYD NCHUNGA BIHARAGU.
Nakala kwa:-
Mama Fatma Karume,Mdhamini
Francis Kifukwe, Mdhamini
Bwana Yusuf Manji – Kwa taarifa

LLOYD NCHUNGA BIHARAGU
C/O LLOYD ADVOCATES,
Morogoro/Bibi TIti  Mohamed Rd,7th Floor, J.K. Nyerere Pension towers
P.BOX 75111, Dar-Es- Salaam,Tanzania.

No comments:

Post a Comment