contact

husen

Monday, July 22, 2013

UBAGUZI WAZIDI KUIANGAMIZA CHADEMA


UBAGUZI baina ya vyama vya upinzani uliopata nguvu bungeni wakati wa kuanzisha Kambi Rasmi ya Upinzani chini ya Chadema, umeanza kutafuna chama hicho chenye ushawishi mkubwa kuliko vyama vingine vya upinzani Tanzania Bara.



Uundwaji wa Kambi Rasmi ya Upinzani bungeni, ulitokana na msimamo wa Chadema yenye wabunge wengi bungeni, kukataa kushirikisha vyama vingine vya upinzani, ikiwamo CUF ambayo ilikuwa na idadi ya wabunge wanaotosheleza kuunda Kambi ya Upinzani, lakini imezidiwa kiidadi na Chadema.



Chadema pia ilikataa kushirikiana na NCCR- Mageuzi, TLP, UDP na kuamua kuunda kambi ya wabunge wa Chadema pekee, ambapo kwa busara kwa kuwa CUF pia ingeweza kuunda Kambi ya Upinzani, kambi hiyo ya Chadema ikapewa jina la Kambi Rasmi ya Upinzani bungeni.



Athari za ubaguzi huo zilijitokeza Arusha hivi karibuni, ambapo chama hicho kilionekana kutaka kuongoza halmashauri ya jiji hilo, lakini kikashindwa baada ya kukosa kura mbili tu za TLP, na jana imejidhihirisha wakati wa uchaguzi wa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Uvinza mkoani Kigoma.


Katika siasa za Arusha, baada ya Chadema kutetea viti vyake vinne vya udiwani katika uchaguzi mdogo na uliokuwa muhimu kwa siasa za Chadema, ilifikisha viti 15 kwenye Baraza la Madiwani la Arusha, huku CCM ikibakiwa na viti 12 na TLP viti sita.

Pia Chadema mbali na kuwa na viti hivyo 15, inayo nafasi ya kuongeza kiti zaidi, kwani kuna nafasi moja ya viti maalumu iliyokuwa ikishikiliwa na Rehema Mohamed, aliyetimuliwa mwaka 2011.



Hata hivyo, pamoja na Chadema kuongoza kwa kuwa na viti vingi vya udiwani Arusha, haikuwa na uwezo wa kumweka Meya, kwa kuwa idadi ya madiwani wake ni 16 na kingehitaji zaidi ya kura 17 katika baraza, ili kupata nafasi ya kuongoza halmashauri hiyo.



Hivyo Chadema ilihitaji kushirikiana na TLP, ili kupata zaidi ya nusu ya kura inayohitajika kikanuni kumuweka Meya madarakani.



Uvinza Baada ya Chadema kusema haina uroho wa madaraka katika umeya wa jiji la Arusha, chama hicho kimejikuta katika mazingira kama ya Arusha,  mkoani Kigoma. 

Mkoa wa Kigoma, katika halmashauri mpya ya Uvinza, Chadema ikishindwa kuishawishi NCCR-Mageuzi kuwaunga mkono, itakuwa katika mazingira ya kukosa nafasi ya kuongoza halmashauri hiyo mpya.

Katika halmashauri hiyo, CCM ina madiwani wanane, Chadema madiwani saba na NCCR-Mageuzi inayo madiwani watano na Mbunge mmoja, ambaye anaingia katika Baraza la Madiwani na anaruhusiwa kupiga kura na hivyo chama hicho kuwa madiwani sita.



Naibu Katibu Mkuu wa Chadema na Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Kabwe Zitto (Chadema) alinukuliwa akiwataka madiwani wa Chadema na NCCR- Mageuzi, kuunganisha nguvu ili CCM iunde Kambi ya Upinzani katika halmashauri hiyo.


“Chadema na NCCR-Mageuzi tuna madiwani 13 katika Halmashauri ya Wilaya Uvinza…CCM ina madiwani wanane tu, hivyo tuna kura nyingi upinzani. Chadema ina madiwani saba, NCCR-Mageuzi watano na Mbunge mmoja,” alinukuliwa Zitto akishawishi huku akisema wakishindwa kuungana, CCM itapita katikati.

 
Umoja wavunjika Tofauti na matazamio ya Zitto, kwamba vyama hivyo vingeweka mgombea mmoja dhidi ya mgombea wa CCM, Hamisi Mkwafi, NCCRMageuzi pamoja na kuwa na madiwani sita tu, ilisimamisha mgombea wake, Fidelis Kumbo, na Chadema ikaamua kuweka mgombea wake, Cassiano Mabondo.



Katika mazingira yaliyoonesha kuwa vyama hivyo vya upinzani, ikiwemo Chadema vilikuwa na uroho wa nafasi ya Mwenyekiti, havikusimamisha mgombea katika nafasi ya Makamu Mwenyekiti, ambayo CCM ilijikuta ikiwa haina mpinzani baada ya kumsimamisha Diwani wa Kalya, Lucas Kanoni.

Awamu ya kwanza ya uchaguzi huo uliokuwa ukisimamiwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Uvinza, Nicolous Kombe na Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila, ulishindwa kupata mshindi baada ya kila chama kupata kura saba.

Matokeo hayo yaliamsha mjadala wa muda mrefu na mwishowe walikubaliana uchaguzi huo urudiwe, ambapo matokeo yake yalionesha kuwa wajumbe walipigia kura wagombea wa vyama vyao kwani mgombea wa CCM, aliongoza kwa kupata kura nane na kufuatiwa na mgombea wa Chadema aliyepata kura saba na wa NCCR -Mageuzi aliambulia kura sita.

 
Utata Baada ya matokeo ya uchaguzi wa raundi ya pili, mjadala uliibuka tena kuhusu matakwa ya kikanuni, kwamba mshindi anapaswa kupata zaidi ya nusu ya kura za wajumbe waliopiga kura, ambazo ni 11, jambo ambalo hakuna mgombea hata mmoja aliyefikisha.

Msimamizi wa Uchaguzi, Kombe alilazimika kusitisha mjadala huo kwa muda, ili wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi wapate ufafanuzi wa kisheria, kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI).



Baada ya zaidi ya saa moja ya kusubiri, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya Kigoma, Miriam Mbaga, alisema majibu waliyopata yanaeleza kuwa aliyeshinda kwa kura nyingi, mgombea wa CCM Mkwafi, anapaswa kutangazwa mshindi.

Majibu hayo ya Mkurugenzi yalizua tafrani ambapo baadhi ya madiwani walimtaka Mkurugenzi huyo kufuta kauli hiyo, kwa madai kwamba si kauli rasmi.



Mkurugenzi huyo alilazimika kufuta kauli hiyo, na baadaye Msimamizi wa Uchaguzi, Kombe aliahirisha uchaguzi huo hadi utakapoitishwa upya. 


Baada ya kuahirishwa kwa uchaguzi wa Mwenyekiti, wajumbe walikataa kupiga kura kumchagua Makamu Mwenyekiti, ambayo ilikuwa na mgombea mmoja, Kanoni (CCM).

No comments:

Post a Comment