contact

husen

Monday, May 21, 2012

WAZEE WAMNG'OA NCHUNGA

Wanachama  wa klabu ya Yanga, jana kwa kauli moja walitangaza kuung’oa

 madarakani uongozi wa Lloyd Nchunga katika mkutano uliofanyika

 kwenye Uwanja wa Kaunda, jijini Dar es Salaam.

Katika mkutano ulioratibiwa na Baraza la Wazee kwa

 kushirikiana na vijana na kudumu kwa saa 2 nzima,

 ulihamia kwenye uwanja huo kutokana na idadi kubwa ya

 wanachama waliojitokeza kuamua hatima ya klabu yao.

Katika mkutano huo uliodumu kwa saa mbili, kuanzia majira ya

 saa 6 hadi 8 mchana, muda ulivyokuwa ukisogea

, ndivyo wanachama walivyokuwa wanaongezeka.

Ingawa mkutano huo ulianza na wanachama wapatao 556

, lakini hadi unafungwa, walikuwa wamefikia 700,

 wote kwa pamoja wakiridhia kuuweka

 kando uongozi wa Nchunga.

Baada ya mkutano huo kufunguliwa na dua na sala,

 Katibu wa Wazee, Ibrahim Akilimali, alitoa maneno

 machache kuelezea udhaifu wa uongozi wa

 Nchunga tangu uingie

 madarakani Julai 18, 2010.

Akilimali aliwaeleza wanachama kuwa, kutokana na

 mambo kutokwenda sawa katika klabu yao, ndiyo maana

 waliamua kuchukua jukumu la kuitwaa timu kuelekea mechi ya Simba.

Alisema, sababu ya wao kufikia hatua hiyo, ni wachezaji kukosa

 ari ya kucheza kutokana na matatizo ya uongozi wa Nchunga

 ikiwemo kutolipwa mishahara, hivyo kuishi kwa dhiki kubwa.

Akilimali alisema, udhaifu na matatizo ya uongozi wa Nchunga,

 yanathibitishwa na wajumbe wa Kamati ya Utendaji

 walioamua kumsusia klabu hiyo. 

Alisema, miezi michache tangu kuingia madarakani, makamu

 wake, Davis Mosha alijiuzulu akifuatiwa na wajumbe wengine wa

 Kamati ya Utendaji hivi karibuni, hivyo hafai kubaki Yanga.

Mbali ya Mosha, wengine walioachia ngazi, ni Seif Ahmed, Ally Mayay,

 Edgar Chibula na Abdallah Bin Kleb, ambao wote walifanya hivyo

 kutokana na matatizo yaliyomo kwenye uongozi wa Nchunga.

Kuhusu fedha za kuendesha timu, Akilimali alisema tayari 

wameahidiwa kupewa sh mil 750 na watu wenye mapenzi

 na klabu hiyo, na kwamba kuna mfanyabiashara mmoja

 ameahidi kutoa sh mil 250, hivyo kufikia sh bil 1.

Kati ya waliopewa nafasi ya kusema machache, ni kipa

 wa zamani wa timu hiyo, Hamisi Kinye na beki Bakari Malima

 ‘Jembe Ulaya’, ambao waliushutumu uongozi wa

 Nchunga kwa usajili mbovu.

Kwa mujibu wa Katiba ya Yanga, iwapo theluthi ya

 wanachama watajiorodhesha na kutia saini zao,

 maamuzi watakayofikia, ni halali.

Baada ya kupitisha uamuzi huo, Akilimali alisema watawasilisha

 orodha ya wanachama waliojiorodhesha kushiriki mkutano

 huo kwa Msajili wa Vyama na Klabu za Michezo

 Wilaya ya Ilala kuomba uchaguzi mkuu.

Tangu Yanga ipoteze mwelekeo wa ubingwa wa Ligi Kuu,

 kumekuwa na harakati za kuung’oa uongozi wa Nchunga

 kwa hoja ya kushindwa kazi, huku wachezaji na makocha 

wakilia kutolipwa mishahara.


No comments:

Post a Comment