contact

husen

Monday, July 22, 2013

POLISI MKOANI MWANZA YAFAFANUA KWA KINA KUHUSU VIELELEZO VYA KESI VILIVYOIBIWA KITUONI HAPO


WATU wasiofahamika idadi yao wanaodhaniwa wezi, wameiba vielelezo katika stoo ndogo ya Kituo Kikuu cha Polisi Kati, Wilaya ya Nyamagana, mkoani Mwanza baada ya kuvunja madirisha.

Tukio la wizi huo lilifanyika Julai 15, mwaka huu, majira ya usiku wa kuamkia Jumatano katika jengo la Polisi Wilaya ya Nyamagana.

Akizungumza na gazeti la MAJIRA jana, Kamanda wa Polisi Mkoa Naibu Kamishna wa Polisi (DCP) Ernest Mangu, alisema wezi hao kabla ya kuingia ndani ya jengo hilo, walivunja dirisha la ofisi za Elimu, Ukaguzi Kanda ya Ziwa na walipofanikiwa kuingia ndani, walivunja dirisha na kuingia kwenye ofisi za Polisi Nyamagana na kutanua nondo kwa jeki na kisha kuingia kwenye stoo ndogo ambamo vielelezo hivyo vilitunzwa na kuiba begi moja la nguo na kompyuta mbili mpakato.

Moja ya kompyuta hizo ni kielelezo katika kesi ya ujambazi ambayo mtuhumiwa alikamatwa nayo, ambaye kwa sasa yuko mahabusu katika Gereza Kuu la Butimba.

Kamanda Mangu alisema kompyuta ya pili ni kielelezo cha kesi ya uharibifu wa mali inayomkabili fundi mmoja na begi la nguo ambazo mwenye nazo hafahamiki. 



Begi hilo liliokotwa na polisi baada ya kuwakurupusha wezi hao waliokimbia na kulitelekeza.

Alieleza kuwa eneo walikopitia wezi hao usalama wake ni mdogo kwani ni uchochoroni na hakuna ulinzi wala mwanga wa taa, hivyo wanajaribu kuangalia kuboresha usalama wa hapo na maeneo jirani.

No comments:

Post a Comment